TOFAUTI KATI YA MFANYABIASHARA NA MJASIRIAMALI

Kuna mkanganyiko ambao hufanya vijana wengi kushindwa kutofautisha kati ya mfanyabiashara na mjasiriamali. Hawa ni watu wawili tofauti kabisa, mjasiriamali ni mbunifu au mtoa wazo la Biashara linaloweza kuzalisha Bidhaa. Lakini mfanyabiashara ni mtu anayeuza bidhaa iliyokwisha zalishwa na mjasiriamali kwa lengo la kupata faida.

Wote wanategemeana hivyo mmoja asipokuwepo mwingine anaweza kupoteza kabisa mwelekeo wake. Kwa hiyo mjasiriamali lazima ashirikiane na mfanyabiashara katika kutimiza lengo mahususi la muhusika.

Na kila wakati lazima utambue ya kwamba Ujasiriamali una kanuni ambazo unapaswa kuzijua ili kutengeneza au kuzalisha Kitu chenye ubora, ila katika Biashara kazi kubwa ni kuangalia uhitaji wa soko na idadi ya Wateja.
Msingi wa awali wa Mjasiriamali ni wazo, lakini msingi wa kwanza wa mfanyabiashara ni Pesa ya mtaji. Kila Mjasiriamali ni mfanyabiashara lakini si kila mfanyabiashara ni mjasiriamali.

Mjasiriamali ni mtu mwenye imani katika kila jambo analofanya na pia mtu aliyetayari kufanya maamuzi bila ya kujali sana matokeo (risk taker)

Mjasiriamali anatabia ya kufanya Kitu anachokipenda na ndio maana huwa vigumu kukata tamaa hata kama kukitokea changamoto kiasi gani. Ni mtu jasiri na anaethubutu kufanya vitu ambavyo wengine huviogopa kuvifanya.

Na zaidi mjasiriamali ana nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya muda pesa na mali zake. Tofauti na mfanyabiashara akipata pesa ya ziada ni lazima aongeze matumizi na starehe zisizo na ulazima.

Zipo kanuni za Ujasiriamali ambazo Mjasiriamali lazima azifuate ili afanikiwe.

1. Lazima awe mbunifu (Innovative)

Hii ni tabia kubwa muhimu ambayo kwa kila mjasiliamali yeyote yule lazima awe nayo, bila ubunifu kwa hicho unachokifanya Ni bure. Ubunifu si kutengeneza kitu awali/ au Ni kitendo cha kufanya maboresho.

Kwa mfano utaona kila siku kampuni fulani za utengenezaji simu, kila kukicha wanafanya ubunifu kwenye bidhaa zao, hufanya hivyo ili kuongeza wateja. Kama ilivyo katika utengenezaji wa simu tumia kanununi hiyo hiyo katika kuboresha vitu ambavyo unavitengeneza au kuvifanya kwa wateja wako.

Ubunifu upo katika aina 3

A) ubunifu katika kuendeleza na kuboresha bidhaa au huduma yako iliyopo tayari sokoni (innovation in process)

kama unafanya vizuri katika bidhaa au huduma ni lazima uendelee kuboresha zaidi ili kulinda wateja wako na kukidhi matakwa ya wateja wako na huduma yako au bidhaa kuwa na Vifungashishio bora,

B) Ubunifu katika Uzalishaji wa bidhaa au huduma (innovation in product or service)

Mjasiriamali lazima awe mjanja kujua soko la huduma na bidhaa linataka nini uendane na soko usibaki nyuma ya soko, ili kuweza kuhilimili ushindani unaokuwa kila siku, na kuweza kumridhisha mteja (your product or service should satisfies customers need and demand) kama ni mama ntilie hakikisha chakula yako inamvutia mteja kila siku.

kama ni bidhaa ya vinywaji, Nguo, kama ni fundi, Dereva, mwalimu, au chochote kile kinachohusu bidhaa au huduma hakikisha mteja wako unampa bidhaa au huduma itakayomlazimu kurudi kwako tena kutokana na ubunifu wako.

C)Ubunifu katika Usimamizi na Uendeshaji wa taasisi za kazi (innovation in management and work organization) kwa lugha ya kisukuma tunasema hivyo…

inawezekana unaendesha kampuni au taasisi katika uzalishaji wa bidhaa au huduma ubunifu ni muhimu katika usimamizi na kuendesha taasisi au kampuni kwa rasirimali watu ili Taasisi au kampuni ikue kutoka hatua ya chini hadi juu katika uzalishaji au utoaji wa huduma….

Zipo kampuni au Taasisi zimeanzishwa lakini zimekufa, zingine zipo dormant, zingine zinazalisha chini ya kiwango, vyama vya ushirika vimekufa, zingine zipo kama hazipo zote hizo Taasisi, kampuni au taasisi zinahitaji ubunifu katika usimamizi na uendeshaji wake…

2. Nidhamu.
Mjasiriamali yoyote lazima awe na nidhamu na kazi yake, Muda, Pesa inayopatikana kwenye shughuli yake. Wapo wajasiriamali wengine wamechukua mikopo ili kuendesha biashara yao lakini hawana nidhamu na matumizi ya fedha katika kazi yao.

Mjasiriamali ni lazima ajinyime na kujibana ili kufikia malengo makubwa ya kazi yake. Ipo biashara nyingi za wajasiriamali zimekufa na zingine zimeshindwa kukua kutoka chini hadi juu kutokana na ukosefu wa nidhamu ya muda na fedha.

3. Sehemu (place)
Mjasiriamali lazima ujue eneo unalotaka kufanya shughuli zako za Ujasiriamali na mahitaji ya bidhaa au huduma hiyo katika eneo hilo kwa maana (demand) kwa wateja wako katika eneo unalotaka kufanya shughuli za Ujasiriamali wako.

Mfano huwezi kufungua kiwanda cha kinywaji cha Ulevi kwenye Maeneo ya watu wenye Imani na matumizi ya vinywaji vya Ulevi, kwa hiyo lazima eneo hilo liwe na uhitaji wa huduma au bidhaa hiyo unayotaka kufanya.

4. Bei ya bidhaa yako au huduma (price)
ni lazima iendane na thamani ya bidhaa au huduma maana bei ya bidhaa au huduma inaweza kumvuta mteja au kumfukuza mteja hivyo ni lazima bei ilingane na thamani ya huduma au bidhaa kwa wateja wako.

Thamani Kubwa na Nzuri ya huduma au bidhaa utengeneza mazingira ya kumvuta mteja na mteja hujikuta anaridhika na bei hiyo hata kama ni kubwa kwamba ubora wa simu, gari,dawa, vyakula, samani, huduma yako kama ni salon, Mc, Mwalimu, Daktari n.k utengeneza mazingira ya kumridhisha mteja na bei ya huduma au bidhaa yako.

5.Matangazo ya bidhaa yako au Huduma yako.(Promotion)
mjasiriamali lazima uhakikishe unatengeneza mtandao wa wateja wako kujua bidhaa yako au huduma yako unayozslisha iwe kwa kutumia vyombo vya habari au Teknolojia ya mitandao ya kijamii au njia yoyote ambayo wateja wako watafikiwa na taarifa za upatikanaji wa bidhaa yako na huduma yako.

Haitoshi kama mjasiriamali kutengeneza bidhaa nzuri au kuwa na huduma Nzuri lakini jirani zako hawajui na hawana taarifa ya bidhaa yako au huduma yako ndio maana unaona matangazo ya biashara kwenye vyombo vya habari television na redio kila Mara ndio maana unaona nchi yetu inajitahidi kutangaza vivyutio vya utalii huko kwenye nchi zingine ili wajue mlima Kilimanjaro upo Tanzania, wajue Tanzania kuna mbuga za wanyama wa kila aina.

Waswahili wana msemo wao kuwa biashara ni matangazo Mjasiriamali lazima utangaze bidhaa yako au huduma yako kwa njia yoyote ili iwafikie wateja wengi kadri iwezekanavyo.

Maneno ya hamasa na kutiana Moyo na historia za watu waliofanikiwa za kutokata tamaa, kujituma, kujiamini, sijui nini haya yote yakuwa na umuhimu na faida pale utakapokuwa umetimiza kanuni za ujasiriamali na biashara yako ili usipoteze fedha zako na mikopo ukauziwa dhamana zako.

Leave a Reply